Tujenge Nyumba Ya Mungu

Tujenge Nyumba ya Mungu ni kikundi kinachojihusisha na huduma ya kimisheni ya ujenzi wa makanisa vijijini pamoja na kusaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu. Huduma hii imejengwa juu ya misingi ya kujitoa kusiko kwa kawaida; nia thabiti ya moyo wa kujitoa kwa kazi ya Bwana kwa njia ya mali zetu, elimu, ujuzi, muda na maombi bila kukoma kama alivyofanya Nehemia.

MADHUMUNI YA KIKUNDI

Dhumuni kuu la Kikundi hiki ni kusaidiana na wachungaji pamoja na washirika wao hususan katika maeneo ya vijijini kufanikisha ujenzi wa makanisa nchini Tanzania ili watu walio na nia ya kumtafuta Mungu wamwabudu katika mazingira rafiki ya ibada. Pamoja na jukumu hilo, kikundi hiki pia kinajihusisha na kusaidia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi ili kuwasaidia kupata mahitaji muhimu hasa ya elimu na hivyo kuwawezesha kufikia ndoto zao katika elimu. 

MAFANIKIO YA KIKUNDI

Tunamshukuru Mungu kwa jinsi ambavyo amekuwa nasi katika huduma hii kwani mbali na kanisa lililojengwa Wilayani Bunda Mkoani Mara mnano mwaka 2021, ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wa 2023 mara baada ya uzinduzi wa huduma hii, tumefanikiwa kukamilisha ujenzi wa makanisa matatu. Tumejenga makanisa ya kiwango bora kabisa katika eneo la Mitengo Wilayani Mtwara na katika vijiji vya Hinju na Nanjedya Wilayani Nanyamba Mkoani Mtwara.

Wakati huo huo ndani ya mwaka 2024, tunayo mipango ya kukamilisha ujenzi wa makanisa mawili huko Wilayani Nachingwea Mkoani Lindi ambapo hadi sasa kazi ya ujenzi inaendelea. Pia katika mwaka huu wa 2024, tumepanga kukamilisha ujenzi wa majengo matano (5) ya muda katika vijiji vinavyopatikana Wilayani Tandahimba Mkoani Mtwara. Haya ni maeneo ambayo hakuna kabisa kanisa na hivyo kujengwa kwa majengo hayo ya muda ndio kutafanya anagalau kwa mara ya kwanza kuonekana kwa majengo ya makanisa katika maeneo hayo ambayo hadi sasa ibada zinafanyikia kwenye nyumba za watu binafsi.

UPATIKANAJI WA FEDHA

Vifuatavyo ni vyanzo vya fedha: 

1. Michango ya hiyari kutoka kwa wanakikundi wenyewe. 

2. Harambee zenye lengo la kutunisha mfuko wa Kikundi

3. Wadau mbalimbali watakaoguswa na huduma ya Kikundi na hivyo kuamua kuchangia kwa hiyari yao wenyewe

Michango yote ya Kikundi hukusanywa kupitia akaunti nambari 20110077511 Jina la Akaunti TUJENGE NYUMBA YA MUNGU Jina la Benki NMB katika tawi la BANK HOUSE.

SIFA ZA MWANAKIKUNDI

Mtu yeyote anaweza kuwa mwanakikundi ilimradi awe na sifa zifuatazo:

  • Awe tayari kuchangia rasilimali zake ili kufanikisha malengo ya Kikundi
  • Awe tayari kutoa mawazo yake kwa lengo la kuwezesha shughuli za Kikundi kuwa endelevu
  • Awe na mzigo moyoni mwake wa kufanikisha shughuli za Kikundi ikiwa ni pamoja na kuleta watu wengine wenye nia ya kufanikisha shughuli za Kikundi
  • Awe tayari kuheshimu mawazo ya wanakikundi wengine
  • Awe na akili timamu, mtu mzima mwenye umri usiopungua miaka 18
  • Awe mtu mwaminifu mwenye maadili mema ya kiroho na kimwili

MSISITIZO

Mtu yeyeto anaweza kujiunga na Kikundi hiki kwa hiyari yake mwenyewe endapo anauwiwa moyoni mwake katika kufanikisha malengo ya Kikundi hiki kwa njia ya mali zake. Unaweza pia kuchangia kufanikisha shughuli za kikundi bila kuwa Mwanakikundi.

Mwanakikundi atakayebainika kuwa na mwenendo usioendana na sifa za mwanakikundi pamoja na maadili mema, mara moja atakosa sifa za kuwa mwanakikundi.

UENDESHAJI WA KIKUNDI

Kikundi kina viongozi waliochaguliwa na wana wajibu wa kutoa taaarifa mbalimbali za maendeleo ya Kikundi ikiwa ni pamoja na kiasi cha pesa zilizochangwa, majina ya wachangiaji pamoja na kuonesha namna fedha zilivyotumika katika shughuli za Kikundi.

Viongozi wa kikundi ni:

  1. Mwenyekiti
  2. Katibu
  3. Mtunza hazina

Viongozi katika nafasi tajwa hapo juu ndio watiasaini wa uchukuaji fedha kutoka kwenye akaunti ya Kikundi kwa ajili ya shughuli za Kikundi.

JINSI YA KUBAINI MAENEO YA KUJENGA MAKANISA

ama ilivyoelezwa hapo awali, huduma hii inahusika na ujenzi wa makanisa maeneo ya vijijini na siyo mijini. Kutokana na ufinyu wa rasirimali fedha, hata huko vijijini bila shaka huduma hii haiwezi kujenga makanisa kila eneo kwa wakati mmoja. Hivyo basi, uongozi wa huduma ya Tujenge Nyumba ya Mungu umeweka vigezo kadhaa ili kurahisisha zoezi la ubainishaji wa maeneo ya kufanyika baraka ya kujenga makanisa. Pamoja na msaada wa mwongozo wa Roho Mtakatifu, vigezo hivyo hutumika kuongoza timu ya wajumbe walioenda kutembelea maeneo husika. Maamzi ya kuchagua eneo la ujenzi hufanywa na timu ya wajumbe hao kisha kushirikisha viongozi wa kikundi na baadaye hushirikisha wanakikundi wote juu ya maamzi yao.

Maeneo yanayochaguliwa kujengwa, siyo lazima ujezi uanze mwaka huo huo. Kulingana na vipaumbele vya kikundi, ujenzi unaweza kufanyika hata miaka kadhaa mbeleni. Ujenzi unaweza kuwa ni wa majengo ya kudumu au ya muda kutegemeana na bajeti au hali halisi ya eneo lililochaguliwa.

MAHALI

Kikundi cha Tujenge Nyumba ya Mungu kinapatikana Kimara – Dar Es Salaam Tanzania.

ANGALIZO

Kikundi hiki hakiruhusu fedha zozote zilizo haramu au michango yenye lengo la kutakatisha fedha kutoka kwa wanakikundi au kwa wadau watakaoamua kuchangia fedha kwa ajili ya kufanikisha shughuli mbalimbali za kikundi. Ikibainika mwanakikundi amefanya hivyo, kikundi hakitasita kutoa taarifa kwa vyombo husika ikiwa ni pamoja na kufutwa uanakikundi.

KWA MAWASILIANO ZAIDI WASILIANA NA

  1. Mwenyekiti 0763 547 281
  2. Katibu 0676 101 125
  3. Mtunza hazina 0754 443 668

WAKFU HUDUMA YA TUJENGE NYUMBA YA MUNGU TAREHE 12/03/2023

MIRADI YA UJENZI WA MAKANISA

MRADI WA UJENZI WA KANISA LA EAGT MITENGO WILAYA YA MTWARA

MRADI WA UJENZI WA KANISA LA TAG HINJU WILIYANI NANYAMBA MKOANI MTWARA

MRADI WA UJENZI WA KANISA LA TAG NANJEDYA WILIYANI NANYAMBA MKOANI MTWARA